Maskani Leo, Jumatatu, Oktoba 7,2024

Maskani Leo Online Edition : maskanileo-254newsday.blogspot.com

a).Tangazo

Ndugu WanaBaze, Maskani Leo imetimiza mwezi mmoja kamili jana tangu tulipoanza kuchapisha mnamo Septemba 6! Imekuwa ni mwezi wa faida kubwa kwa familia ya Apollo Veve Baze (AvB), na tumejivunia kuwatumikia kwa jicho la uanahabari thabiti. Hii ni hatua ndogo lakini yenye athari kubwa kwa WanaBaze. Kwanza kabisa, tunawatangazia kwamba kuanzia leo, kwa kusherehekea hii milestone ya kipekee, Maskani Leo itapatikana pia mtandaoni kupitia tovuti maskanileo-254newsday.blogspot.com, inayopatikana kwa yeyote aliye na intaneti, kote duniani. 


Jina la nembo yetu ya toleo la mtandaoni, kama ile ya toleo la karatasi, linabaki kuwa alama ya umoja wetu — Apollo premium veve! 

b). Yaliyojiri Wikendi...

Haikuwa wikendi ya kawaida hapa AvB. Jumamosi na Jumapili, kama ilivyo kawaida, Apollo Veve Baze ilikuwa ikiwaka moto, na kufika saa sita mchana, hakukuwa na nafasi ya kusimama! Lakini kilichojitokeza sana wiki hii ni wingi wa sura mpya, wageni wapya waliokuja kujiongeza kwenye familia ya WanaBaze inayozidi kuongezeka kwa kasi. Hawa wapya wanakaribishwa kwa mikono miwili! Apollo mwenyewe alisema kwamba kuwakaribisha rasmi pale AvB, kila mmoja anastahili kupata kikombe cha kahawa. Weh! Sio ya kawaida hiyo!

Na ukiwa hapo Baze ukifurahia jaba yako, kumbuka mambo ya maana unayoweza kufaidi kwa urahisi. Kuna AvB Noticeboard, mahali unapata taarifa zote muhimu na matangazo ya wanajamii. Halafu kuna AvB MiniLibrary kwa wasomi na wale wanaopenda kujiongeza maarifa kidogo kidogo. Na bila kusahau, AvB Maskani Leo, gazeti letu la familia, lenye kila kitu utakacho kuhusu maisha ya AvB. Hakika, hapa ni Maskani yenye kila kitu!

c). MwanaBaze Wa Leo

Leo ni Jumatatu, na unajua kinachoendelea... kuna mmoja wetu anayesubiri kubeba zawadi yake ya jaba ya Sh50! Si mwingine bali ni Chege Mwicigi, aliyeshika namba nne kwenye droo ya wiki iliyopita. Mwicigi ni jamaa mchapa kazi, na unamkuta sana pale kituo cha matatu cha Gatura. Sio kwa bahati, maana yeye ni dereva wa matatu kitaalamu anayesaka kazi kwenye sekta ya matatu au hata sehemu nyingine yoyote kama dereva. Hata leseni yake iko tayari, na anasema yuko tayari kuanza kazi haraka iwezekanavyo. Kwa hiyo, kama kuna MwanaBaze yeyote anayemjua mtu anayetafuta dereva, basi Chege Mwicigi anapatikana kupitia nambari 0712889332. Msaada wako unathaminiwa sana!

d). Hongera na Pongezi

Mwisho lakini si kwa uchache, Ngechu, maarufu kama J, jana alitoa msaada wa rimu moja ya karatasi kwa hiari yake ili kuendeleza juhudi za utoaji habari na elimu zinazozidi kukua pale Baze. Huu ni mfano mzuri wa roho ya AvB ambayo Maskani Leo imekuwa ikiihubiri ndani na nje ya Apollo Veve Baze. Tunawaomba WanaBaze wengine wafuate mfano wa Ngechu, ili kila mmoja afaidi kutoka kwa mwingine. Hakika, "kuwa mlinzi wa ndugu yako!" Kwa hilo Ngechu, bila shaka Apollo anakudai kikombe cha kahawa! Yangu ni maoni tu, lakini!

Haya basi, hiyo kiojo tu! Pata kusoma nakala nzima ambayo ni kurasa 7 ya makala motomoto ya kihistoria, habari, maoni na burudani, yote bila malipo katika Apollo Veve Baze! Tupatane hapo githaa. Au siyo??