Maskani Leo, Alhamisi, Okt 3, 2024

 


Alhamisi, Okt 3, 2024

SEHEMU YA 1: MASKANI KWA APOLLO JANA

a). Yaliyojiri

Unajua vile Jumatano huwa siku ya kazi kubwa Gatura Town, manze, ni siku ya soko. Na Apollo Veve Baze (AVB) haikubaki nyuma! Mapema tu baada ya kufunguliwa, WanaBaze wakawa wameanza kujaa – wa kawaida na wale wa wasio - walifurika. Kufikia saa nane, maze, Baze ilikuwa imejaaa hadi capacity. Hata section ya nje, pale kwa wale wanaopenda kustream fresh air na kuenjoy space, hakuna kiti kilikuwa kimebakia! 

Sasa, story ya maana hapa ni kwa Sarah – mrembo wa power (kushoto kwenye picha), sasa ni regular na ni outspoken kama kawaida. Alikuwa kwa mood fiti, akaomba basi picha ya WanaBaze wa nje ipigwe. Kulingana naye, hawajawahi kuonekana kwa Maskani Leo, na vile walikua wamejienjoy inabidi wapate recognition. Sarah, umetuambia, na kama kawaida Maskani Leo iko ready kukufanyia mambo. Tuko hapa kuunganisha familia ya AVB na kufanya kila mtu ahisi ako ndani, na ombi lako limefanyiwa kazi! Au sio?

b). MwanaBaze Wa Leo

Leo ni Alhamisi, siku ya mwisho ya kutambua MwanaBaze Wa Leo kwa wiki hii. Na unajua nani ametoboa leo? Ni John Gitonga Mwai aka Faite! Apollo mwenyewe amesema huyu jamaa ni daily customer, na anasubiria ku-reward jamaa na jaba ya chwani. Hii ni shukrani ndogo tu ya kusema "asante sana kwa kuwa loyal customer wa Baze". Kama kawaida, week ijayo kuna lineup safi ya MwanaBaze Wa Leo! Tunawangoja Mwicigi, Ngucita, na Long watawika Jumatatu, Jumanne na Alhamisi. Lakini Apollo ametuonya – no picha, no reward, hata kidogo! So tuma picha mapema ama uulize kupigwa, ama sivyo utaangukia pande flani.

SEHEMU YA 2: BURUDANI

Kidosho avamiwa na nzi baada ya kupora mihela ya buda gesti - Taifa Leo

WAKAZI wa kijiji kimoja Msambweni walishuhudia tukio la kusikitisha, mwanadada mmoja alipovamiwa na jeshi la nzi saa chache baada ya kuonywa na buda mmoja kwamba angekiona cha mtema kuni kwa kupora pesa zake.

Haikubainika jinsi demu alivyopora pesa za mzee huyo lakini wakazi walishuku walikuwa wakiponda raha katika gesti mmoja. “Watu walisikia buda akimuonya demu kuwa kama hangerudisha pesa zake, angejuta. Dakika chache baada ya kutoa onyo hilo, mzee aliondoka kwa gari lake na demu akaendelea na shughuli zake.”

“Hata hivyo, watu walishangaa alipovamiwa na nzi mwili mzima huku akionekana kutojali,” alisema mdokezi.

Demu alipoulizwa alichomfanyia buda huyo hakuweza kutoa sauti na watu wa familia wakalazimika kumtafuta buda ili kumuokoa binti yao.

Inasemekana walisaka nyumba ya demu wakapata bunda la pesa na kumpelekea mzee ndipo nzi wakaacha kumuandama. SEHEMU YA 3: MAKALA ELEZEA

Ruto anavyomchinja Gachagua kwa kisu alichokificha kwenye tabasamu - Mwananchi

Wakanda ni dola ya kufikirika Afrika Mashariki, ndani ya mfululizo wa vitabu vya Fantastic Four. Shujaa Black Panther ambaye jina lake halisi ni T'Challa, anafanya kila kitu kuhakikisha anailinda dola yake, The Kingdom of Wakanda.

Inawezekana Wakanda ni Kenya. Mchuano mkali ni kiti cha Black Panther. Kutoka Uhuru Kenyatta na William Ruto, sasa Ikulu ya Kenya inawaka moto baina Ruto na naibu wake, Rigathi Gachagua. Kila mmoja anajipambanua kuwa ndiye T’Challa, mtetezi halisi wa Kenya.

Uhuru alipokuwa Rais wa Kenya, alitofautiana na naibu wake, Ruto, namna ya kufikiri kuhusu kesho ya Kenya. Ukaibuka uhasama baina yao. Uhuru akatamba yeye ndiye T’Challa, mtetezi wa Kenya, vivyo hivyo kwa Ruto. Uhuru akasema Ruto ni hatari kwa Kenya, Ruto akasiliba kwamba Uhuru ni msaliti wa Kenya.

Kisha, Kenya ilifanya Uchaguzi Mkuu Agosti 9, 2022. Ruto na Gachagua, walikuwa wagombea jozi. Wakichangia sauti moja. Chuki dhidi ya Uhuru ilikuwa wazi kwenye nyuso na katika matamshi yao. Uhuru akataka T’Challa mpya Kenya baada yake, awe Raila Odinga. Haikuwezekana, Ruto alishinda urais, Gachagua, Naibu Rais.

Kutoka Septemba 13, 2022, Ruto na Gachagua, walipokula kiapo kuiongoza Kenya, ni miaka miwili imetimia, jina la Gachagua lipo kwenye mchakato wa kibunge, wenye hatima ya kumpigia kura ya kutokuwa na imani naye. Swali siyo wamefikaje huku, bali je, Gachagua ataponyoka? 

Kambi ya wabunge wengi Kenya (majority caucus), ndiyo inampitisha Gachagua kwenye machinjio. Wabunge na maseneta wa kambi ya Ruto, wanamwona Gachagua ni kikwazo na hatoshi kuendelea kuwa msaidizi mkuu wa Ruto. Wamedhamiria kumwondoa.

Chokochoko ilianza kama piga nikupige langoni, katika mchezo wa soka. Gachagua alionya wabunge kubaki maeneo yao ya uwakilishi, badala ya kuzuru na kufanya siasa kwenye majimbo mengine. Ruto akawatetea wabunge, wazunguke popote Kenya ili kufanya kazi yao.

Halafu, maandamano makubwa ya vijana, kundi rika la Generation Z, yakazidi kumimina petroli kwenye moto ulioanza kuwaka. Gachagua akakimbilia kwa Uhuru, akasema ni “mtoto wa nyumbani” Mlima Kenya. Ruto akajisalimisha kwa Raila. Gachagua akarusha mashambulizi kwa Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa Kenya, Noordin Haji, Ruto akamtetea.

Kwa mujibu wa mashitaka dhidi ya Gachagua bungeni, kwanza anatuhumiwa kukiuka ibara ya 10 ya Katiba ya Kenya, inayoelekeza katika ibara ndogo ya pili, kuhusu uzalendo, mshikamano wa kitaifa, uadilifu na mengineyo. Gachagua anashutumiwa kwa kufanya siasa za kimaeneo, akiegemea nyumbani kwao, Mlima Kenya.

Gachagua anatuhumiwa na wabunge kwa kukiuka misingi ya kitaifa na utawala, ambayo ndiyo mwongozo wa ibara ya 10 ya Katiba ya Kenya, kwa kuwashambulia viongozi wenzake hadharani, Mkurugenzi wa Usalama (Haji) na Jaji wa Mahakama ya Juu Kenya, Esther Maina.

Kuhusu Haji, Gachagua alisema mkuu huyo wa Idara ya Usalama, amekuwa akimpotosha Rais Ruto, na kushindwa kumpa ushauri mzuri, hasa katika sakata la Generation Z. Upande wa Jaji Maina, alimshambulia kwa kutoa uamuzi dhidi yake kabla hajawa Naibu Rais, kwamba alijipatia Sh200 milioni za Kenya (Sh4.2 bilioni za Tanzania), kifisadi.

Makosa mengine ambayo yamewasilishwa bungeni ni rushwa na kujipatia mali kifisadi. Gachagua anadaiwa kununua hoteli za Treetops na Outspan, zilizopo kwenye Hifadhi ya Taifa ya Aberdare. Nyingine ni hoteli za Olive Gardens na Vipingo Beach Resort, zilizopo Kilifi. Zipo mali nyingine ambazo Gachagua anadaiwa kuzinunua miezi ya karibuni, kinyume na kipato chake.

Hoja ya kutokuwa na imani na Gachagua, imewasilishwa bungeni kwa mujibu wa ibara ya 150 (1) (b) na (2), inayotaka mtoa hoja ya kumwondoa Naibu Rais, lazima athibitishe sababu za msingi kuwa kiongozi huyo anakuwa amevunja sheria za ndani au za kimataifa.

Wabunge wanamtuhumu Gachagua kwa kukiuka sheria mbalimbali za nchi; Sheria ya Mshikamano na Ushirikiano, Sheria ya Mwendelezo wa Uhalifu na Mapambano dhidi ya Utakatishaji Fedha Haramu, Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sheria ya Uongozi na Uadilifu, Sheria ya Kukabiliana na Rushwa pamoja na Uhalifu wa Kiuchumi.

Spika wa Bunge, Moses Wetangula, ameripotiwa kuunga mkono hoja hiyo dhidi ya Gachagua. Kiongozi wa wabunge wengi, Kimani Ichungwah, ameviambia vyombo vya habari kuwa hoja ya kumng’oa Gachagua ni nzito na inajitosheleza.

Wabunge na maseneta kutoka Mlima Kenya, wameungana kutaka Gachagua aondoke, kisha nafasi yake ichukuliwe na Kithure Kindiki, ambaye ni Waziri wa Mambo ya Ndani na Utawala wa Kitaifa. Kabla ya Uchaguzi Mkuu Kenya 2022, wabunge na maseneta wa Mlima, walimpendekeza Kindiki kuwa mgombea mwenza wa Ruto, ambaye aliamua kusimama na Gachagua. Dhahiri, wabunge na maseneta wengi wa Mlima, hawapo na Gachagua, ambaye karata yake ni kwao, Mlima ili kumtisha Ruto. Ilivyo wazi, Gachagua hakukubalika tangu mwanzo Mlima Kenya, ila Ruto alimteua kuwa mgombea mwenza wake, kwa imani kuwa angemtii.

Ni kipindi hiki, Uhuru yupo zake kimya, pengine akicheka kwa kufunika kinywa ili asionekane. Ni kama anasema “kiko wapi”, vishindo vya Ruto na Gachagua, kumshughulikia na familia yake, wameishia kushughulikiana wenyewe.

Timu ya Raila na wapinzani wengine dhidi ya Ruto na naibu wake, Gachagua, wao wanasema “chickens come home to roost” – “ubaya unarejea ulipotoka”. Ushirikiano wa Ruto na Gachagua, haukuundwa kwa misingi ya uongozi wala kwa ajili ya kesho njema ya Kenya, bali manufaa binafsi na masilahi ya ukabila. Hiyo ndiyo gharama.

Wanaona matokeo ya sasa ya Ruto na Gachagua, ni sawa na ilivyotokea kwa Uhuru na Ruto, waliungana kwa sababu wote walikuwa washitakiwa wa kesi ya uhalifu wa kibinadamu, Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC). Hawakupatana kiuongozi wala tamaa ya kuijenga Kenya iliyo bora.

Gachagua amekuwa akiamini kuwa Ruto hatapitisha uamuzi wa yeye kuondolewa kwenye kiti cha Naibu Rais. Anasema, uhusiano wake na Ruto ni wenye afya kabisa, isipokuwa bosi wake huyo amekuwa akipotoshwa na watu wanaomzunguka.

Wakati huohuo, Gachagua analalamika kuondolewa kwenye shajara (diary) ya Rais Ruto, ambayo aliunganishwa kupitia kundi la kimtandao la WhatsApp. Gachagua anaeleza kuwa yeye na wasaidizi wake wa karibu, wameondolewa kwenye kundi hilo la WhatsApp, ambalo ndilo huwekwa ratiba na mipango ya kikazi ya Rais Ruto.

Asichojua Gachagua ni kuwa anachinjwa na Ruto kwa kisu kilichofichwa kwenye tabasamu. Ni kanuni ya Jenerali Wang Jingze, aliyoandika katika sura ya pili ya kitabu “Thirty-Six Stratagems.” Unamkenulia adui, adanganyike kuwa kila kitu kipo sawa, halafu akizubaa, unamchinja. 

HITIMISHO

Mchapishaji: Paul Kimani

Mhariri: askMRMOI

© Maskani Leo ni Chapisho la Apollo Veve Baze, 2024.